Naibu wa gavana wa kaunti ya Nakuru Joseph Ruto amekanusha madai ya baadhi ya watu waliojitambulisha kama wazee wa jamii ya Wakalenjin kuwa Gavana Kinuthia Mbugua anaendeleza ukabila.
Akizungumza na waandishi wa habari afisini mwake Jumatatu, Ruto alisema kuwa madai hayo ni ya uongo na ilitokana na baadhi ya watu wanaotaka kugawanya watu katika misingi ya kikabila katika jimbo la Nakuru.
Siku ya Jumapili, kikundi cha watu kilichojitambulisha kama wazee wa jamii ya Wakalenjin wakiongozwa na Bw Pius Lai walidai kwamba gavana Mbugua alikuwa akiendeleza ukabila na kuwatenga watu kutoka jamii ya Wakalenjin katika ugavi wa rasilimali katika kaunti.
“Bw Lai sio mwenyekiti wa chama cha wazee wa jamii ya Wakalenjin na hana mamlaka yoyote ya kuzungumza kwa niaba yao, ninayemtambua anajulikana kama Bw Josiah Ruto,” alisema naibu wa gavana.
Ruto aliongeza kuwa halikuwa jambo la busara kwa Lai kutoa matamshi ya uchochezi haswa ikizingatiwa kuwa kuna mzozo unaoendelea kati ya jamii za Wakalenjin na Wamaasai katika maeneo ya Naivasha kwa sasa.