Naibu Rais William Ruto ameyapinga madai ya baadhi ya viongozi wa kanisa nchini kuwa serikali inapanga kuwakandamiza wahubiri kulingana na sheria mpya iliyochapishwa na mamlaka ya mawasiliano nchini (CAK) juma lilopita.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumapili alipoungana na waumini wengine katika kanisa la Jesus Celebration Centre (JCC) Bamburi, naibu rais alisema kuwa serikali inatambua uhuru wa kuabudu na hivyo haiwezi wanyima wahubiri fursa ya kueneza neno la Mungu kwa Wakristo.

Hata hivyo, Ruto alisema kuwa sheria hiyo inalenga kuwafungia nje baadhi ya wahuburi wanaolitumia jina la Mungu kuwahadaa na kuwalaghia waumini na kisha kujinufaisha.

“Kuna baadhi ya wahubiri wanaotumia jina la Mungu vibaya. Wao sasa hawana nafasi katika jamii. Huweza ambia mtu apande mbegu eti ndio abarikiwe. Jameni tuhubiri neno na tuache ukora na ulaghai,” alisema Ruto.

Ruto pia alizua ucheshi kanisani aliposema kuwa wahuburi wanaotaka waumini wapande mbegu ili wabarikiwe watalazimika kujisajili na kampuni ya mbegu chini 'Kenya Seed Company' (KSC) kabla kuruhusiwa kufanya hivyo.

Wiki iliyopita, mamlaka ya mawasiliano nchini (CAK) ilichapisha sheria mpya kwa vyombo vya habari kuhusu suala la mahuburi ya redio na runinga.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, hakuna muhubiri atakayeruhusiwa kuomba sadaka wala kuwalazimu waumini na uokovu.

Viongozi wengi wa kanisa walipinga vikali sheria hiyo, lakini Ruto amewaahidi kuwa serikali itaitathmini tena na kisha kuvifanyia marekebisho vipengee tata kabla kuanza kutumika rasmi.