Naibu rais William Ruto amesema kuwa Luke Kimutai Samoei aliyetajwa kwenye sakata ya NYS na aliyekuwa waziri wa ugatuzi Ann Waiguru sio ndugu yake.
Katika taarifa, Ruto kupitia kwa katibu wake wa Mawasiliano David Mugonyi hata hivyo amevikosoa baadhi ya vyombo vya habari kwa kukosa kudhibitisha uhalali wa madai hayo yaliyotolewa kwenye hati kiapo iliyotolewa na Bi Ann Waiguru mapema wiki hii.
Hati ya kiapo ya Waziri huyo wa zamani iliwataja aliyekuwa naibu Mkurugenzi mkuu wa NYS Adan Harakhe, Waziri wa Fedha Henry Rotich na Luke Kimutai Somoei anayedaiwa kuwa nduguye naibu rais ambapo alidai kuwa walihusika pakubwa katika kubana ukweli kuhusu sakata hiyo.
Wengine waliotajwa ni kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wote wakiwa tayari wamejitenga na tuhuma hizo.