Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu wa Rais William Ruto amewataka viongozi wote kutoka eneo la Pwani kushirikiana na serikali ya taifa ili kuleta maendelea na kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo hayo.

Ruto amesema kuwa iwapo kila kiongozi atatia bidii kuboresha maisha ya wakazi kwa ushirikiano wa serikali, uchumi wa maeneo hayo utaimarika zaidi.

Ruto, ambaye alikuwa akiongea katika mji wa kwale kwenye ziara rasmi ya serikali siku ya Ijumaa aliwataka viongozi kupunguza siasa na kuwahudumia wananchi na kuwahusisha wakazi katika miradi ya kuinua hali ya maisha yao.

Ruto aliongeza kuwa serikali ya Jubilee inajitahidi kuleta miradi ya serikali katika kila kaunti bila mapendeleo yoyote, na kudokeza kuwa yeye na Rais Kenyatta watahakikisha kuwa ahadi zote walitoa kwa wananchi zitatimia.

Ruto, ambaye alizuru wilaya tofauti katika eneo zima la Pwani aliwapongeza kina mama pamoja na vijana kwa juhudi zao za kujaribu kuimarisha viwango vya uchumi katika maeneo hayo.

Naibu rais pia aliweza kufungua rasmi kituo cha polisi cha Vigurungani katika eneo bunge la Kinango, ambapo alikuwa ameandamana na maafisa mbalimbali kutoka serikali kuu pamoja na viongozi wengine kutoka Pwani akiwemo gavana wa Kwale Salim Mvurya.

Kiongozi huyo alichukua nafasi hiyo kutetea serikali dhidi ya madai ya ufisadi, huku akisema kuwa serikali ipo na ukakamavu wa kupigana na hongo na ufisadi kwa jumla kwenye idara tofauti, na watawajibikia kila shilingi ambayo imetengwa miradi mbali mbali.