Serikali ya jimbo la Nakuru imewataka viongozi kukomesha matamshi yanayolenga kuchochea wakazi kisiasa haswa kwenye mikutano ya hadhara, na badala yake kuendeleza amani kwa umoja wa taifa la Kenya.
Wakiongozwa na naibu gavana wa jimbo la Nakuru Joseph Ruto, wamesema kuwa kumezuka mizozo katika kipindi cha miezi miwili iliyopita katika maeneo tofauti ya jimbo la Nakuru, na iwapo wanasiasa hawawajibiki, huenda ikapelekea migawanyiko ya kikabila katika jimbo.
Ruto, akiongea Nakuru mjini Jumatatu alisema ikizingatiwa Kenya imeshuhudia mauaji kutokana na tofauti za kisiasa na mizozo ya kikabila, inasikitisha bado kuna matamshi ya kiholela yanayotokana na viongozi wasiojali maslahi ya wakenya.
Alisema kati ya maeneo yaliyoathirika ni ikiwemo Mau Narok, Mauche, Ol-posimoru na sasa Naivasha kutokana na matamshi sawia na hayo yanayotoka kwa viongozi.
“Hatuwezi kubali kurudishwa na watu wachache wenye matakwa yao ya kibinafsi na kisiasa katika mauaji kama ya 2007, tunahitaji kuishi pamoja kama familia moja ya Kenya,” alisema Rutto.