Seneta wa kaunti ya Nyamira Mong'are Okong'o amejitokeza kuwaomba wakazi wa kaunti ya Nyamira kuwekeza pakubwa katika masuala ya elimu ili kuwasaidia vijana kujiendelesha.
Kwenye kikao na wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa, Mong'are alisema kutokana na kutokuwepo ardhi ya kutosha Gusii, jamii hiyo inaweza tu kujistawisha iwapo wakazi wataekeza pakubwa kwenye elimu.
"Inajulikana wazi kwamba hatuna ardhi ya kutosha Gusii kwa sababu ya idadi ya watu inayoendelea kuongezeka, na iwapo tunataka kustawi sharti tuekeze pakubwa katika elimu," alisema Mong'are.
Mong'are aidha alishtumu vikali ajira za watoto kwa kile alichosema tabia hiyo huwazimia watoto wengi ndoto zao huku akiwaonya wahusika kuchukiliwa hatua za kisheria.
"Ni onyo kwa wale watu walio na mazoea ya kuwapa ajira watoto, na wacha wajue kuwa yeyote atakayepatikana atakabiliwa vikali kisheria kwa maana ajira za watoto huwazimia ndoto maishani," aliongezea Mong'are.