Seneta wa Kaunti ya Nyamira Okongo Mong'are amemshutumu vikali spika wa bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko kwa kuongoza ujumbe wa wawakilishi wadi kwenda nyumbani kwa naibu Rais William Ruto huko Sugoi mapema mwezi huu.
Akihutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumanne, Mong'are alisema spika Nyamoko alikosea pakubwa kuwaongoza wawakilishi wadi kwenye safari hiyo, huku ikizingatiwa wengi wao ni wanachama wa mlengo wa Cord.
"Inawezekanaje kwamba spika Nyamoko anaweza waongoza wawakilishi wadi zaidi ya kumi ambao ni wa mrengo wa Cord kuelekea nyumbani kwake Ruto kule Sugoi na kwa hakika hilo ni kosa," alisema Mong'are.
Mong'are aidha alihoji wajumbe hao hawakuwakilisha maoni na matakwa ya wananchi kwenye safari hiyo ila walienda kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
"Asije mtu akawadanganya wananchi kwamba ujumbe uliosafiri kwenda Sugoi ulienda huku ili kuwasilisha matakwa ya wakazi wa eneo hili ila nia yao ilikuwa ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa ila wacha wajue Nyamira ni ngome ya Cord," aliongezea Mongare.