Seneta wa kaunti ya Nyamira Mong'are Okong'o anaitaka serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kusuluhisha mzozo wa kimpaka eneo la Keroka kwa njia ya amani. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea na mwanahabari huyu siku ya Alhamisi, Mong'are alisema kuwa yafaa serikali za kaunti hizo mbili ziketi na kusuluhisha mzozo huo wa kimpaka ili kustawisha utangamano. 

"Naona wakati umefika kwa serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kuketi pamoja na kusuluhisha mzozo wa kimpaka wa eneo la Keroka kwa maana tunalohitaji ni kustawisha utangamano," alisema Mong'are. 

Mong'are aidha alisisitiza kwamba eneo hilo la mzozo liko katika himaya ya kaunti ya Nyamira, ila akawasihi wananchi kutochukua sheria mikononi mwao kwa kuwa hali hiyo huenda ikasababisha umwagikaji damu.

"Kwa mara nimekuwa nikipata ripoti kwamba wananchi wa eneo hilo huwafurusha kwa nguvu watoza ushuru wa kaunti ya Kisii, ningewaomba wawe watulivu kwa maana hatuhitaji kuona aina yeyote ya umwagikaji damu, na ninalojua ni kuwa mji wa Keroka upo katika kaunti ya Nyamira," aliongezea Mong'are. 

Haya yanajiri baada ya serikali za kaunti hizo mbili kuendelea kuzozona kuhusiana na eneo hilo la Keroka huku kila moja ikidai kuwa mji wa Keroka upo katika kaunti yao. 

Picha: Seneta wa kaunti ya Nyamira Mong'are Okong'o. Anaitaka serikali ya kaunti ya Nyamira na ile ya Kisii kusuluhisha mzozo wa kimpaka eneo la Keroka kwa njia ya amani. Maktaba