Seneta mteule Martha Wangari ameonya kuwa huenda ufisadi uliokithiri serikalini ukalemaza juhudi za serikali ya Jubilee.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea Jumanne mjini Naivasha alipozindua mradi wa maji, Wangari alisema kuwa ufisadi umekithiri serikalini na maafisa wakuu serikalini wanahusika. 

 Wangari amemtaka rais Uhuru Kenyatta kufanya juhudi na kumaliza ufisadi ulio serikalini. 

"Iwapo Rais Kenyatta hatachukua hatua basi huenda miradi mikubwa iliyoanzishwa na serikali ikakwama kutokana na ukosefu wa fedha," alisema Wangari. 

"Mradi wa reli ya kisasa huenda usifaulu kwa sababu kila afisa serikalini anataka kuiba pesa na hii itaangamiza Jubilee," aliongeza.

Seneta huyo wa chama cha UDF aliwashutumu wabunge wa muungano wa Jubilee aliosema wamekaa kimya huku serikali ikiporwa na maafisa wake. 

"Wabunge wa Jubilee wamejawa na unafiki kwa sababu hawataki kusema ukweli na wanawakinga wezi serikalini. Maafisa wengi wamehusika na wizi lakini wabunge wanawatetea kwa sababu wanakula nao," alisema.

Aliwataka Wakenya na haswa mashirika ya kijamii kuwa macho na kushinikiza serikali kutoa taarifa kamili kuhusiana na ufisadi unaoripotiwa.