Siku chache tu baada ya seneta Okong'o Mong'are kuteuliwa mwenyekiti wa kamati ya uhasibu wa pesa za umma PAC kwenye bunge la seneti na kisha kufurushwa na chama cha Cord kwa kushukiwa kuwa mfisadi na kutokuwa mwaminifu kwa chama, sasa seneta huyo amejitokeza kusema yungali mwenyekiti wa kamati hiyo maana alichaguliwa kwa huru na haki.
Akiwahutubia wanahabari mjini Nyamira siku ya Ijumaa, Mong'are alisuta hatua huku akiitaja kama ya ubinafsi mkubwa hali aliyosema inaua demokrasia nchini.
"Nilichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya PAC kwa njia ya huru na haki na hata seneta wa Kakamega Bonny Khalwale akanipongeza kwa kumpiku, na hatua ya seneta Muthama kunichuja ni ubinafsi mkubwa ambao nia yake ni kuangamiza demokrasia nchini," alisema Mong'are.
Mong'are aidha aliyasuta madai ya kuwa mfisadi, huku akimtaja seneta wa Machakos kama kiongozi fisadi zaidi huku akimpa changamoto kutangaza mali yake wazi na jinsi alivyo yapata.
"Baadhi ya wanachama wa Cord wamenitaja kuwa mfisadi eti ndio sababu hawana nia ya kuniruhusu kuhudumu kwenye kamati ya uhasibu ila swali langu ni hili, huyu Muthama anaweza waeleza wakenya jinsi alivyopata mali yake," aliuliza Mong'are.