Bunge la seneti lina umuhimu mkubwa katika maswala ya ugatuzi humu nchini na halifai kuvunjiliwa mbali.
Ni usemi wake mwenyekiti wa ODM Nakuru Dennis Okomol ambaye anasema kuwa ni jambo la kusikitisha kuwepo shinikizo za kuvunjilia mbali bunge hilo.
Kwa mujibu wake, iwapo bunge hilo la seneti litavunjwa, basi ugatuzi utakuwa umeuawa humu nchini.
Akizungumza Alhamisi wakati wa kikao na wanahabari, Okomol aliwataja wabunge wanaoshinikiza kuvunjiliwa mbali kwa seneti kama maadui wa mabadiliko.
“Hao wabunge hawajawai kubali kwamba seneti ndilo bunge kuu nchini ndiposa wanataka kuangamiza ugatuzi,” alisema Okomol.
Wakati huo huo, ametoa wito kwa serikali kuhakikisha kwamba nafasi za uteuzi wa wabunge maalumu kama vile wawakilishi wa walemavu zinasalia.
Anasema kuwa nafasi zote za uongozi zilizo kwa katiba ni za umuhimu, ndiposa wananchi walipasisha katiba hio.