Share news tips with us here at Hivisasa

Bunge la kaunti ya Uasin Gishu linapania kubuni sera ambayo itawahamasisha wakulima kuhusu umuhimu wa kuanza kukumbatia kilimo cha matunda na mboga.

Sera hiyo inalenga kuhimiza wakulima kuhusu kilimo mbadala baada ya kubainika kwamba uzalishaji wa nafaka umerudi chini kutokana na ongezeko la tindikali mchangani.

Tayari bunge la kaunti hiyo limeidhinisha hoja kuhusu sera hiyo ambayo iliwasilishwa bungeni humo na mwakilishi wadi Tembelio Pius Kigen.

Kigen alisema iwapo sera hiyo itafaulu wakulima wataboresha mapato yao kutokana na kilimo kinyume na ilivyo kwa sasa ambapo mapato yao yamerudi chini kutokana na ongezeko la Tindikali mchangani.

“Wakati umefika kwa wakulima wetu kuelezewa umuhimu wa kuanza kupanda mboga na matunda kwa wingi ikizingatiwa faida yake kinyume na kilimo cha mara kwa mara cha nafaka,” alisema  Kigen

“Kulingana na Kigen ni kwamba matumizi ya mara kwa mara ya mbolea zenye kemikali kwa upanzi wa mahindi na ngano yamechangia kwa kina ongezeko la tindikali mchangani hivyo basi rutupa ardhini imerudi chini,” alisema

Kigen alitaka wadau katika sekta ya kilimo katika kaunti ya Uasin Gishu kushirikiana na bunge hilo katika uhamasisho kuhusu sera hiyo.

“Itakuwa vyema zaidi iwapo wadau wote watashirikiana katika uhamasisho huu, ikizingatiwa kuwa ongezeko la tindikali mchangani imefanya mavuno kurudi chini. Kilimo cha mboga na matunda kinafaidi faida bora ikilinganishwa na nafaka," alisema.

Kiongozi huyo alisema kuna soko tele la kilimo cha mboga na matunda hasa matunda aina ya karakara ambayo yana soko katika masoko ya kimataifa.

Mwakilishi wadi huyo alitaka wakulima husika kutumia vilivyo nafasi ya kusafirisha mazao hayo katika mataifa ya kigeni kwa kutumia uwanja wa Ndege wa kimatiafa wa Eldoret.