Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA kaunti ya Nakuru Abdul Noor amemwomba waziri wa ugatuzi Mwangi Kiunjuri kushughulikia maslahi ya wakimbizi wa ndani katika kaunti za Nakuru na Nyandarua kwa kuwapa fidia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Noor alikuwa akizungumza siku ya Alhamisi jijini Nakuru baada ya kuandaa mkutano na baadhi wa wakimbizi hao ambao ni waathirika wa vita vya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008.
"Tunamwomba waziri Kiunjuri kuwapa fidia au kuwapa makazi mapya wakimbizi zaidi ya 15,000 ambao wanaendelea kuumia katika makambi yao katika kaunti za Nakuru na Nyandarua. Ni jambo la kusikitisha kuona serikali bado haijatimiza ahadi yao kwa wakimbizi hawa huku uchaguzi ujao ukikaribia," Noor alielezea.
Noor pia amedokeza kuwa wakimbizi hao wana kila haki ya kuishi kwa amani kama wakenya wengine nchini bila kubaguliwa.
"Serikali inahitaji kufahamu kuwa watu hawa pia walipiga kura zao ili kuchagua viongozi wao na pia wanatarajia kushiriki katika usajili wa kuchukua kura ili wapige kura mwaka ujao. Kila mmoja ana haki ya kupiga kura katika mazingira mema bila kuwekewa vikwazo vyovyote," Noor ameelezea.
Kwa upande wake, naibu katibu wa muungano wa wakimbizi nchini John Njoroge ameitaka serikali kutuma watu ambao watafika katika maeneo hayo kushuhudia maisha ya wakimbizi ili kufahamu mazingira wanayoishi.
"Imekuwa mda sasa tangu serikali iahidi kushughulikia wakimbizi na tumechoka kusubiri ahadi hizo tena. Ni wakati serikali inafaa kuwajibika na kusaidia wakimbizi nao pia wapate kuishi maisha mema," Njoroge alisema.