Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwakilishi wa Wanawake katika Kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa amedai kuwa serikali ina njama ya kuwaangamiza kisiasa kutokana na kuwa muungano waliokuwa nao wa kisiasa Malindi huenda ukachangia serikali iliyoko madarakani kwa sasa kubanduliwa.

Akizungumza siku ya Ijumaa katika mkutano na wanahabari, Jumwa alisema kuwa hatua ambayo serikali ilichukua ya kumpokonya Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho walinzi wake, huenda ikasababisha hatari kubwa kwani kiongozi huyo atakuwa anatekeleza majukumu yake bila ya ulinzi.

Kiongozi huyo wa wanawake alisema kuwa mshirikishi mkuu wa utawala katika kanda ya Pwani Nelson Marwa anafaa kuwajibikia majukumu yake badala ya kuingilia viongozi wa kisiasa na kusababisha uhasama usiofaa kwa jamii.

Jumwa alieleza kuwa ni jukumu la idara ya usalama kuwapa viongozi ulinzi na iwapo wanawapokonya kwa madai ya kuwa walinzi wao walitumia mamlaka yao vibaya kuwakandamiza wakaazi, basi hatua inafaa kuchukuliwa dhidi ya walinzi hao, badala ya kuwapokonya viongozi walinzi.

“Nadhani sheria ipo wazi kuwa mtu akifanya kosa anachukuliwa hatua ama kuonywa lakini kutupokonya walinzi hiyo nikutuweka katika hali ya hatari na mahasidi wetu wa kisiasa, kwa sababu wanaweza kutumia nafasi hiyo kutuandama,” alisema Jumwa.

Kiongozi huyo kwa sasa anaitaka serikali kuwapa ulinzi kwani hatua hiyo huenda ikawaletea shida na kuwapelekea kushindwa kutembea maeneo ya mbali.