Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali imeahidi kufungua vituo vingine vipya vya huduma kwa wananchi katika ngazi ya kaunti ndogo nchini ili kurahisisha shughuli za utoaji wa huduma za umma kwa wakazi wa mashinani.

Akiwahutubia wakazi katika kituo cha Huduma mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kamishna wa kaunti hiyo Nelson Marwa alisema kwamba tayari serikali imeandaa mikakati mwafaka ya kuidhinisha vituo hivyo katika kila kaunti ndogo ili kuona kwamba wakazi wananufaika na mradi huo.

Kulingana na Marwa, kituo hicho kimesaidia pakubwa wakazi waliokuwa wakipitia changamoto nyingi za kupata vyeti vya kitaifa, na hatua hiyo inafaa kuungawa mkono zaidi ili kupunguza misongamano na kucheleweshwa kupata vyeti hivyo muhimu.

Aidha, amewahimiza wakazi kufika katika kituo hicho na kuchukua vyeti vyao vya kitaifa walivyotuma maombi ili kupunguza msongomano wa vyeti hivyo katika afisi za kituo hicho, kwani wakazi wengi waliyotuma maombi ya kupata vyeti vya kitaifa bado hawajavichukua.

"Serikali imeandaa mikakati mwafaka ya kuimarisha huduma kwa wananchi inapatikana kwa urahisi, na sasa iko mipango ya kufungua vituo vingine zaidi katika kila kaunti ndogo ili kuona kwamba mwananchi wa mashinani anapata huduma hii," alisema Kamishna Marwa. 

Hata hivyo, wakazi waliokuwa katika kituo hicho walielezea kuridhishwa kwao na hatua ya serikali ya kurahisisia majukumu kwa wananchi ya kutafuta vyeti vya kitaifa ikiwemo kitambulisho na stakabadhi zingine muhimu.

Kamishna huyo wa kaunti amewahimiza maafisa wa kituo hicho kuimarisha uhusiano mwema na wakazi wakati wa utoaji wa huduma hiyo ili kuona kwamba mpango huo wa serikali unafanikiwa.