Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali yake itafanya kazi na vijana ili kusaidia kutatua shida zinazokumba taifa la Kenya. 

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akijibu maswali kuhusu ulanguzi wa dawa za kulevya, ardhi na ufisadi katika ikulu ya Mombasa siku ya Jumatano alipoandaa kikao cha ulizwaji na ujibizaji maswali kilichohudhuriwa na vijana zaidi ya 600 kutoka Mombasa, Rais alisema ana imani kuwa kufanya kazi na vijana hao kutachangia kupatikana kwa suluhu kwa baadhi ya changamoto nchini. 

"Jameni tufanye kazi pamoja tujenge taifa letu, tusiwe watu wa kulalamika kila mara. Tuwe watu wa kukabili shida na kutoa suluhu,'' alihimiza Rais. 

Kenyatta vilevile aliwaahidi vijana hao kuwa yeyote atakayetoa taarifa muhimu kwa serikali kuhusu ulanguzi wa mihadarati na visa vya ufisadi hatodhulumiwa bali atapewa usalama wakutosha. 

Rais pia alisema kuwa vituo vya kurekebisha tabia vitajengwa mjini Mombasa pamoja na Lamu ili kusaidia kuwarekebisha vijana ambao wameathirika kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. 

Kuhusu vyeti vya taifa Rais Kenyatta aliwataka maafisa husika kuharakisha utoaji wa vitambulisho kwa vijana ili kuwaepusha na unyanyasaji mikononi mwa maafisa wa polisi.

Akizungumza kwenye kikao hicho, waziri wa usalama wa ndani Joseph Nkaissery aliwahimiza vijana kujiepusha na makundi haramu na badala yake wajihusishe na ujenzi wa mataifa.