Waziri wa Vijana, jinsia na huduma za umma nchini Bi Sicily Kanini Kariuki amesema kuwa serikali itakakikisha kuwa huduma zote za umma zinatekelezwa vyema.
Akizungumza na wanahabari baada ya kutembelea kituo cha Huduma Center mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Bi Sicily amesema kuwa wakazi wanaopokea huduma za serikali katika kituo hicho wanadai kupokea huduma bora licha ya kuwa na uhaba wa maafisa.
Amesema kuwa serikali itahakikisha kuwa vituo vya huduma za umma vinafunguliwa hadi mashinani ili kupunguza msongamano katika kituo hicho na wananchi kupata huduma zote za serikali kwa urahisi na haraka.
Wakati uo huo amewahakikishia wakazi wa Pwani kuwa hitilafu za kimitambo katika vituo vya huduma za umma nchini zilizoshuhudiwa kwa muda wa majuma matatu sasa zimerekebishwa licha ya kuwepo na changamoto katika utoaji wa vyeti vya kitaifa ikiwemo vitambulisho.
"Kama serikali tumetatua hitilafu yote ya kimitambo na sasa huduma zetu zimerejea kama kawaida kwa hivyo mambo ya kutafuta vitambulisho sasa iko sawa Wakenya wanaweza kufuatilia," alieleza Sicily.
Ameahidi kuwa Serikali itahakikisha kuwa changamoto zote wanazopitia wananchi katika kutafuta huduma za serikali zitakabiliwa na huduma hizo zitatolewa hadi mashinani.