Serikali itajenga vyuo vya kiufundi katika eneo bunge la Likoni na Changamwe mjini Mombasa, ili kutoa nafasi kwa vijana ambao hawajahitimu kujiunga na vyuo vikuu kupata mafunzo ya kiufundi katika kozi mbalimbali.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi katika hafla ya kutoa hati miliki kwa maskwota wa shamba la waitiki, Naibu Rais William Ruto alisema serikali imetenga shilingi laki milioni 100 ili kufanikisha shughuli hiyo.
"Tunataka vijana wetu wajifunze kazi za mkono ili wajisaidie kimaisha, kama serikali hatutaki kuwaona vijana wetu wakihangaika mitaani bila kazi ya kufanya wakati wanaweza jitegemea kimaisha," alisema Ruto.
Ruto aliongeza kuwa vyuo hivyo vitasaidia kupunguza visa vya vijana wengi kujiunga na makundi haramu baada ya kukosa matumaini maishani kufuatia kuchanganyikiwa na ugumu wa maisha.
Ukosefu wa ajira kwa mara nyingi umetajwa kama chanzo cha vijana wengi mkoani Pwani kujiunga na makundi ya uhalifu.