Serikali imeahidi kukamilisha mradi wa ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa ili kuhakikisha kuwa shughuli za uchukuzi zinafanyika kwa urasihi na kuboresha sekta ya utalii.
Akizungumza na wanahabari baada ya kufanya mazungumzo ya kina na wasimamizi wakuu wa shirika la huduma za feri nchini ikiwemo mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Musa Hassan Musa pamoja na Waziri wa Utalii nchini Najib Balala, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutapunguza msongamano katika kivuko cha feri cha Likoni.
Rais Kenyatta alizuru kwa mara ya kwanza tangu mvutano kuhusu huduma duni katika kivuko hicho kuanza kushuhudiwa, na amesema kuwa shida ambazo wakazi wanaotumia kivuko cha feri cha Likoni wamekuwa wakipitia lazima zisitishwe kwa kuboreshwa kwa huduma za feri.
“Tunawaomba wakenya waotumia kivuko cha feri kuwa na subri kwa sababu mikakati mwafaka imeidhinishwa kusitisha changamoto za kivuko cha feri na tayari mradi wa ujenzi wa barabara ya Dongo Kundu inakamilika hivi haribuni ili kuhakikisha kuwa wakazi wanatumia feri na magari kuelekea na barabra hiyo,” alieza Rais siku ya Jumatatu katika afisi za shirika hilo eneo la Likoni mjini Mombasa.
Aidha amewahimiza wasimamizi wa shirika hilo kuwajibikia majukumu yao ipasavyo ili kuzuia kutoshuhudiwa kwa majanga katika kivuko hicho, huku akisema kuwa kushuhudiwa mara kwa mara hitilafu za kimitambo huenda ikasababisha hasara na lazima swala hilo kushughulikiwa.