Share news tips with us here at Hivisasa

Kama njia moja ya kukabiliana na changamoto zinazokumba wasichana kama vile matatizo ya hedhi ambayo huwafanya wnegi kukosa kuhudhuria shule, serikali ya kaunti ya Nakuru kupitia mwakilishi wa ofisi ya gavana Peter Mbae, imepokeza wasichana wasiopungua 300 sodo za kuwasidia katika hali hiyo.

Wasichana hao wa shule za msingi na upili kutoka kila jimbo la Nakuru wamekuwa wakihudhuria semina katika kanisa la Kibaptisti eneo la Solai wilayani Nakuru Kaskazini.

Kulingana na kasisi wa kanisa hilo Stephen Tirop, kuna haja ya kuleta kizazi cha sasa pamoja na kuwapa ushauri, haswa wakati huu ambapo vijana wameanza kujiingiza katika anasa za mapema.

“Inasikitisha kwamba watoto wadogo wamekosa heshima, wanaingia vilabuni kunywa pombe, kufanya ngono na kuvuta dawa za kulevya. Jamii yetu itapotoka zaidi kama kanisa hatutawashikilia” akasema mhubiri Tirop.

Hata hivyo Tirop alishukuru serikali ya kaunti kwa msaada huo huku akiyataka mashirika mengine yajitokeze na kutoa kuwasaidia watoto kutoka jamii maskini na familia ambazo zimekumbwa na changamoto za kimaisha.

Baadhi ya wasichana waliozungumza na mwandishi huyu walielezea furaha yao.

“Tungetaka msaada huu pia uwe ukitolewa shuleni kwani wengi wetu hukusa kuhudhuria masomo kutokna na ukosefu wa sodo,” akasema Mary Wambui.