Wakulima wanaofuga kuku kwenye kaunti ya Nyamira wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kaunti hiyo kuanza kuwapa mafunzo wakulima hao kuhusiana na mbinu mpya za kufanya kilimo hicho.
Kulingana na afisa wa uzalishaji wa mifugo kwenye wilaya ya Nyamira Kaskazini Kennedy Kenyanya, tayari serikali ya kaunti hiyo imeanzisha mchakato wa kuwatuma maafisa watakaopeana mafunzo hayo kwenye kaunti ndogo tano za kaunti ya Nyamira ili kufanikisha shughuli hiyo.
"Tayari maafisa wataalam wa ufugaji kuku wametumwa kwenye kaunti zote ndogo za kaunti hii ili kuwapa mafunzo wakulima wanaofuga kuku ili kuwasaidia kuimarisha biashara zao zaidi," alisema Kenyanya.
Afisa huyo ameongeza kwa kusema kuwa wakati umefika kwa wakulima wanaofuga kuku kwa matumizi yao ya nyumbani kuanza kufuga kuku hao kwa minajili ya kuwauza ili waweze kuimarisha mapato yao.
"Kwa muda sasa watu wengi wamekuwa wakiwafuga kuku kwa matumizi yao ya nyumbani lakini sasa wakati umewadia kwa wakulima hao kuanza kufuga kuku wa kuuzwa ili waweze kuimarisha mapato yao," aliongezea Kenyanya.
Kwa upande wake mkulima mmoja aliyenufaika na mfunzo hayo kutoka wadi ya Bokeira Agnes Ondabu, anatumai kutumia mafunzo ya maafisa wa nyanjani ili kuimarisha ufugaji kuku wake.
"Nitatumia mafunzo niliyoyapata kutoka kwa maafisa wa nyanjani ili niweze kuimarisha kilimo cha ufugaji kuku kwa kuwa natumai mapato yangu yataimarika hata zaidi," alisema Ondabu.