Mshauri wa kifedha katika Benki ya Dunia tawi la Kenya ameitaka serikali ya Kaunti ya Nyamira kutotumia kesi iliyoko mahakamani baina ya halmashauri ya KeRRA, na baraza la magavana nchini, kama kizingiti kinachowafanya kutokarabati barabara katika kaunti hiyo.
Akihutubu katika eneo la Mecheo siku ya Jumapili, Charles Mochama alisema kuwa barabara nyingi zinazostahili kukarabatiwa na serikali ya kaunti bado hazijakarabatiwa kutokana na serikali ya kaunti kuendelea kuisingizia halmashauri ya mpito TA, kama kikwazo cha kutoanzishwa kwa miradi hiyo.
Mochama alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Nyamira inafaa kukarabati barabara mashinani bila ya kungoja msaada wa serikali kuu.
"Tunajua barabara zilizoko chini ya serikali za kaunti na zile zilizoko chini ya KeRRA. Ni jambo la kushangaza kwamba barabara nyingi ziko katika hali mbaya. Serikali ya kaunti inastahili kuacha kuwadanganya wananchi kuwa barabara hizo ziko chini ya serikali ya kitaifa," alisema Mochama.
Mochama aidha aliishtuma idara ya barabara na kazi za umma kwenye kaunti hiyo kwa kutotafuta namna ya kufanya kikao na wabunge wa eneo hilo, ili kuafikia mwafaka wa jinsi barabara hizo zitakavyo karabatiwa.
Mochama alitishia kuchapisha majina ya barabara zilizoko katika hali mbaya ili kuishurutisha serikali ya kaunti hiyo kuzikarabati.
"Idara ya barabara na kazi za umma imekuwa ikizembea badala ya kutafuta namna ya kufanya kikao na wabunge wa eneo hili, ili kuafikiana jinsi ya kukarabati barabara za eneo hili. Itanilazimu kuchapisha majina ya barabara zilizoko katika hali mbaya kisha nishurutishe serikali ya kaunti hii kuzikarabati," aliongezea Mochama.