Share news tips with us here at Hivisasa

Wasimamizi katika makao ya watoto ya Mama Ngina jijini Kisumu, wamesema wao hukabiliwa na changamoto si haba, katika mchakato wa kuwahakikishia maisha bora watoto walio kwenye makao hayo.

Naibu wa msimamizi wa makaazi ya watoto ya Mama Ngina jijini Kisumu Ruth Odhiambo, alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa magari ya kuwasafirisha watoto kutoka kwenye makao hayo hadi shuleni, hospitalini na safari nyingine muhimu.

Alisema kuwa wakati mwingine, huwa vigumu kwao kuwasafirisha watoto hadi hospitalini, hasa wanapokua wagonjwa majira ya usiku.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi, Odhiambo alitoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Kisumu na serikali kuu kutoa msaada kwa makao hayo, ili kuwawezesha kuafikia mahitaji ya watoto kikamilifu.

“Tunakabiliwa na changamoto si haba. Hatuna blanketi, magodoro na blanketi za kutosha miongoni mwa mahitaji mengine,” alisema Odhiambo.

Kauli ya Odhiambo iliungwa mkono na mmoja wa wafanyakazi katika makao hayo Rose Ngeso, ambaye alisema wao hufanya kazi kwa muda mrefu, lakini wanapata mshahara duni.