Mwenyekiti wa muungano wa wanawake Waislamu mjini Mombasa, Farida Rashid, ameilaumu serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kile alichokitaja kama kutowapa ulinzi wa kutosha watoto wanoa randaranda mitaani, dhidi ya ubakaji na dhuluma zinginezo.
Akizungumza afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mwanaharakati huyo wa masuala ya kifamilia, alisema kuwa watoto wengi hususan wa kike wanao randaranda mtaani humo, hupitia dhuluma mbalimbali ikiwemo kuhangaishwa na maafisa wa mji nyakati za usiku.
Alisema kuwa baadhi yao hulazimishwa kushiriki ngono na wanaume wanaowatishia kuwapiga iwapo watadinda kuliitikia hitaji lao.
“Watoto hawa pia wana haki kuishi kama watoto wengine, hivyo hatufai kuwapuuza. Lazima serikali ya kaunti iwahakikishie usalama na iwalinde dhidi ya unyanyasaji,’’ alisema Rashid.
Rashid sasa ameitaka serikali ya kaunti ya Mombasa kuweka mikakati thabiti ikiwemo kuwapeleka watoto hao katika vituo vya kuwalinda watoto yatima, kama njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa haki zao zinalindwa.
Kauli ya Rashid inajiri mwezi mmoja tu tangu watoto wanao randaranda mitaani mjini Mombasa kulalamika kuwa wanahangaishwa na askari wa miji nyakati za usiku, kwa madai kuwa wao ni wezi.