Serikali ya kaunti ya Nyamira imejitenga vikali na madai kuwa inalifadhili kundi la vijana kuwahangaisha watu wanaopinga sera za serikali ya kaunti hiyo.
Kulingana na katibu wa kaunti hiyo Erick Onchana, madai kama hayo hayana msingi, huku akiwasihi vijana wanaoibua madai hayo kuandikisha ripoti kwa polisi, la sivyo serikali ya kaunti hiyo iwapeleke mahakamani kujibu mashtaka.
“Serikali ya kaunti hii haina ufahamu kuwa kuna genge linalowahangaisha wapinzani wa sera za gavana Nyagarama, na madai kama hayo ni ya uongo na yasiyo na msingi na yenye nia yakuiharibia jina serikali ya kaunti ya Nyamira,” aliongezea Onchana.
Onchana aidha amesema kuwa watu wanaoshukiwa kuwa genge la kuhangaisha wapinzani wa gavana Nyagarama ni madereva wa idara mbalimbali za serikali ya kaunti hiyo ambao hawana afisi zao rasmi, hali inayowalazimu kukaa nje ya afisi kuu za kaunti kuwasubiri wakubwa wao.
“Mimi huwanaona madereva wanaowangoja wakubwa wao kwenye maeneo ya kuegeza magari nje ya jengo kuu la serikali ya kaunti na ni jambo la kushangaza kuwa madereva hao wanaweza shukiwa kuwa genge la kuwahangaisha wapinzani wa gavana Nyagarama,” aliongezea.
Haya yanajiri baada ya muungano wa vijana mjini Nyamira almaarufu ‘Nyamira Youth for Change’ kuiandikia barua serikali ya kaunti hiyo kutaka kujua kazi za watu ambao hukaa nje ya jengo kuu la serikali ya kaunti hiyo na ambao humwandama gavana Nyagarama kokote aendako na kuchukua majukumu ya maafisa wa ulinzi.