Mwaniaji wa ubunge kwenye eneo bunge la Kitutu Masaba Shadrack Mose ameishtumu serikali ya kaunti ya Nyamira kwa kushindwa kukarabati barabara kwenye eneo bunge hilo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akihutubu kwenye eneo la Miriri wakati alipotembelea kundi la maendeleo ya vijana wa Miriri, Mose alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nyamira imeshindwa kuafikia matakwa ya wakazi wa eneo hilo, hasa Wakulima, huku akiongeza kusema kuwa serikali ya kaunti hiyo ilitenga eneo hilo pakubwa kuhusiana na kukarabatiwa kwa kilomita 240 za barabara kwenye kaunti nzima ya Nyamira.

“Serikali ya kaunti hii imeshindwa pakubwa kuafikia matakwa ya wakazi wa eneo hili hasa Wakulima, na kwa kweli eneo hili halikufaidi sana kutokana na mradi wa serikali ya kaunti kukarabati kilomita 240 za barabara kote Nyamira," alisema Mose.

Mose aidha aliongeza kusema kuwa kutokana na hali mbaya ya barabara za eneo hilo, inawawia vigumu wakulima kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, huku akiisuta serikali ya kaunti kwa kutoweka kando pesa za kukabili majanga katika eneo la Kitutu Masaba.

“Inawawia vigumu sana wakulima kusafirisha mazao yao kwenda sokoni, na huu ndio wakati mwafaka wa kutumia pesa zilizotengwa kukabili majanga ya El-nino kwa kuwa mvua kubwa inayoendelea kunyesha imeathiri pakubwa barabara za eneo hili,” aliongeza Mose.