Wakazi wa wadi ya Esise wana kila sababu ya kutabasamu baada ya serikali ya kaunti ya Nyamira kununua mitambo miwili ya maji ya kunyunyizia mashamba katika eneo hilo. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi mradi huo kule Nyansiongo siku ya Jumapili, mwakilishi wa wadi ya Nyansiongo Jackson Mogusu aliipongeza serikali ya kaunti ya Nyamira kwa kununua pampu hizo zitakazosaidia kusambaza maji kutoka kidimbwi cha maji yaliyoko karibu, huku akiongezea kusema kuwa hali hiyo itawasaidia wananchi wa sehemu hiyo kupata maji kwa urahisi. 

"Nina furaha sana kwamba hatimaye serikali ya kaunti imesikiza kilio chetu na sisi sote tunaunga mkono maendeleo, na nina hakika kuwa mpango huu utawasaidia wakazi wa eneo hilo kupata maji kwa urahisi," alisema Mogusu. 

Mogusu aidha aliwaomba wakazi wa eneo hilo kuhifadhi maji hasa kwenye msimu huu wa mvua ili kujiandaa kwa msimu wa kiangazi mapema mwaka ujao. 

"Lazima tujipange kuhakikisha kuwa tunahifadhi maji hasa kwenye msimu huu wa mvua na sio tu kutegemea maji ya mifereji kwa kuwa msimu wa kiangazi unakaribia," alihimiza Mogusu. 

Kwa upande wake naibu afisa msimamizi wa maji Francis Oyaro, serikali ya kaunti ya Nyamira iko imara kuhakikisha maji yanapatikana kwa urahasi na wananchi wote wananufaika. 

"Tumetambua maeneo ambayo yanahitaji huduma za maji kwa sana, na tayari tumeweka mikakati kuhakikisha kuwa maji hayo yanapatikana kwa urahisi na wakazi wote wanafaidi," alisema Oyaro.

Pampu hizo zilizo nunuliwa kwa kima cha shillingi elfu 300,000 zitasaidia kusambaza maji kwenye shule na zahanati mbalimbali kule Borabu.