Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nyamira imeombwa kujenga shule ya walemavu katika kaunti ya Nyamira ili kuwasaidia watu wanaoishi na ulemavu kujifunza taaluma mbalimbali na kujisaidia katika siku za usoni.

Ombi hilo limetolewa baada ya kubainika kuwa hakuna shule ya walemavu katika kaunti ya Nyamira.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Nyamira, mwenyekiti wa watu wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Nyamira, Nyaundi Nyaosi, aliomba serikali ya kaunti kujenga shule ya walemavu katika kaunti hiyo kama njia moja ya kuwasaidia watu wanaoishi na ulemavu kujiimarisha kimaisha.

“Shule ya walemavu inastahili kujengwa hapa Nyamira ili waweze kupokezwa mafunzo ambayo yatawasaidia kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha,” alisema Nyaosi.

Aliongeza, “Ikiwa serikali ya kaunti inataka kusaidia watu wanaoishi na ulemavu kupata elimu na kupunguza umaskini, sharti iwajibike kwa kujenga shule ya walemavu hapa Nyamira.”

Aidha, mwenyekiti huyo aliwashauri watu wanaoishi na ulemavu kutotegemea pesa za kuomba omba katika mitaa, na kusema kuwa wana uwezo wa kufanya kazi.

“Hakuna haja ya watu wanaoishi na ulemavu kusema hawawezi kufanya kazi. Lazima kila mtu ajitolee kufanya kazi ili kupata riziki ya kila siku badala ya kutegema pesa za wengine,” alisema Nyaosi.