Mwakilishi wa wadi ya Kiamokama eneo bunge la Nyaribari Masaba kaunti ya Kisii Kennedy Maina ameiomba serikali ya kaunti ya kisii kutumia pesa zilizotengwa kukabiliana na kupambana na El Nino ili kutoa usaidizi kwa wanaothiriwa na mvua hiyo.
Wito huo umetolewa baada ya vyoo vya shule ya upili ya Mobamba na ile ya Ibacho kuzama mnamo siku ya Jumanne, na kuacha wanafunzi bila vyoo.
Akizungumza na waandishi wa habari mnamo siku ya Jumatano katika shule ya Mobamba, mwakilishi huyo alisema serikali ya kaunti ya Kisii ilitenga pesa za kukabiliana na mvua ya El Nino, na kuna haja ya pesa hizo kuanza kutumika mara moja ili kujenga vyoo vya shule hizo viilivyozama.
“Tunaomba serikali ya kaunti ijenge vyoo vya shule hizi maana sisi wawakilishi wa wadi katika kaunti ya Kisii tulipitisha mswada wa millioni 50 ili kupambana na changamoto zitakazosababishwa na mvua ya El Nino,” alisema Maina.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule ya Ibacho Zablon Oginda, maafisa wa afya kutoka kaunti ya Kisii walipotembelea shule hiyo waliagiza vyoo hivyo kujengwa kwa wiki mbili ili kuimarisa hali ya afya, la sivyo shule hizo zifungwe .
“Naomba serikali itusaidie ili tujengewe vyoo 18 jinsi tuliagizwa na maafisa wa afya ili tusifungiwe shule,” alisema Oginda.