Serikali ya kaunti ya Nyamira imetenga shillingi millioni mbili, pesa zitakazosaidia kukarabati zahanati ya Mwongori na kuinua hadhi yake kuifanya kuwa hospitali kubwa. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akiongea alipoitembelea hospitali hiyo siku ya Jumapili, katibu wa wizara ya afya Douglas Bosire alisema kuwa ukarabari huo utaanza kwa wiki chache zijazo. 

"Tunaendelea kuweka mikakati ili kuhakikisha kuwa kuna angalau hospitali mbili za 'level four' katika kila kaunti ndogo kwa minajili ya kupunguza misongamano ya wagonjwa inayoshuhudiwa kwenye hospitali kuu ya Nyamira, na Mwongori ni mojawapo ya hospitali tunayotaka kuinua hadhi yake kwa wiki chache zijazo kwa kuweka vitanda vya kutosha ili isaidie watu wengi," alisema Bosire. 

Afisa huyo aliongeza kwa kusema kuwa zahanati hiyo itakuwa na wadi za kina mama za kujifungua, na pia wadi ya watoto zitakazojengwa kupitia ufadhili wa serikali ya kaunti ya Nyamira kwa ushirikiano na shirika la Dr Joy Foundation. 

"Ili kuifanya iwe hospitali ya kisasa, serikali ya kaunti ya Nyamira itashirikiana na shirika la Dr Joy foundation kujenga wadi ya watoto na ya akina mama kujifungua ili iwasaidie wakazi wa eneo bunge la Borabu kupata huduma za matibabu karibu na nyumbani," alisema Bosire. 

Mradi huo utakapokamilika utakuwa miongoni mwa hospitali ya Nyansiongo, Matongo na ile ya Keroka ambazo zimepandishwa hadhi yakuwa hospitali za level four kwenye kaunti ya Nyamira.