Balozi wa Marekani nchini Robert Godek amesema kuwa serikali ya Marekani itaendelea kuunga mkono masuala ya elimu, na itashirikiana na serikali ya Kenya kuinua viwango vya elimu.
Godek ameongeza kusema kuwa Marekani ina mpango wa kuimarisha mifumo yote ya kueneza habari kwa raia kama vile makitaba na vituo vya kutoa elimu kupitia mitandaoni.
Akiongea katika eneo la majengo na waandishi wa habari siku ya Jumanne kwenye hafla ya kufungua maktaba ya chini ya ufadhili wa serikali ya Marekami maarufu kama American Corner, balozi huyo alisema kuwa hiyo ni hatua moja ya kuwapa nguvu na maarifa vijana wa nchi ya Kenya na kupanua njia za upataji habari kupitia katika vituo kama hivyo vya kujitanua kwa masuala ya ujuzi.
Balozi huyo alionyesha kuridhika kwake jinsi nchi ya Kenya imekuwa ikishughulikia masuala ya kiusalama hasa vita dhidi ya magenge ya kigaidi pamoja na itikadi kali miongoni mwa vijana, na kuahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana kwenye sekta ya usalama na kupigana vikali dhidi ya itikadi kali na makundi ya Al Shaabab.
Balozi huyo atakuwa katika jiji la Mombasa kuendeleza majadiliano na viongozi mbalimbali kutoka kaunti hiyo, na pia atakutana na raia wa Marekani ambao wanaishi katika Kaunti hiyo kujadili masuala ya utalii na uwekezaji.