Mbunge wa Njoro Joseph Kiuna ameihimiza serikali kufutilia mbali madeni yote ya kampuni ya pareto.
Katika mahojiano na wanahabari huyu siku ya Ijumaa mjini Nakuru, mbunge huyo alisema kwamba madeni ya kampuni ya pareto yametokana na wakurugenzi na mameneja wafisadi.
Aliongeza kwamba bodi ya kampuni hiyo inafaa kujumuisha wakulima kutoka kwa maeneo yanayokuza pareto ili waweze kuhisi kana kwamba wanamiliki kampuni hiyo.
Amesema kuwa sio sawa kwa serikali ya Jubilee kukosa kuangazia maswala ya wakulima wa pareto nchini muda wake utakapofikia tamati.
Huku akishukuru kwa juhudi ambayo serikali imefanya kuunga mkono kilimo cha chai, kahawa na miwa, Kiuna amesema kuwa sekta ya pareto inaweza kuwa na nafasi bora ya kuchangia pakubwa katika ukuaji wa uchumi wa Kenya kutokana na hali nzuri ya anga nchini na soko kubwa la bidhaa zinazotokana na zao la pareto duniani.
Wiki iliyopita, wakulima kutoka maeneo yanayokuza pareto chini ya mwavuli wa wakuzaji wa pareto wa eneo la Aberdare waliandikia Rais Uhuru Kenyatta barua wakitaka maslahi ya wakulima wa pareto yaangaziwe.