Ukosefu wa mashini za kutibu ugonjwa wa Saratani katika hopitali kuu ya ukanda wa Pwani imekuwa changamoto kubwa katika kukabiliana na ugonjwa huo kufuatia ongezeko la idadi ya wagonjwa wanaougua ugonjwa wa saratani.
Kwenye mahojiano ya kipekee na mwanahabari huyu katika Hopitali ya Coast Hospices mjini Mombasa, Daktari mkuu katika hospitali hiyo Erick Amis alisema kuwa kuna haja ya serikali kununua mashini maalum za kutibu ugonjwa huo katika hospitali kuu ya ukanda wa Pwani ikiwemo Radio therapy.
Daktari Amis alliongeza kuwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaougua magonjwa ya saratani ni akina mama wanaogua saratani ya kizazi, na kuna haja ya masuala muhimu kuangaziwa.
"Tunaiomba serikali na wafadhili mbalimbali kusaidia kununua vifaa maalum vya kutibu magonjwa ya saratani ili kuhakikisha kuwa magonjwa hayo yanakabiliwa vyema," alisema Amis.
Hata hivyo, ameitaka Wizara ya Afya nchini na zile za kaunti kushirikiana katika kununua vifaa maalum vya kutibu magonjwa ya saratani sambamba na wafadhili wa madawa ili kusaidia kukabiliana na magonjwa hayo.