Mbunge wa Jomvu Badi Twalib ameitaka serikali kuingilia kati swala la mzozo wa ardhi katika maeneo ya Kalahari, Bagladeshi, Aldina na Maganda katika eneo bunge hilo ili kupata suluhu la mzozo huo.
Akiwahutubia wakazi wa eneo bunge lake huko Jomvu mjini Mombasa siku ya Jumatatu katika harambee ya kuchangisha pesa za miradi ya kimaendeleo, Badi alisema kuwa mzozo wa ardhi katika eneo hilo limekithiri mno, na kuna haja ya serikali kuingili kati na kusuluhishwa swala hilo ili kuizuia migogoro na kufurushwa kwa wakazi katika ardhi hizo.
Amesema kuwa tume ya kitaifa ya ardhi nchini chini ya Mwenyekiti wake Mohammed Swazuri walizuru ardhi hizo, lakini hakuna suluhu lolote limepatikana huku wakazi wakizidi kuhangaishwa na baadhi ya watu wanaodai kumiliki ardhi hizo.
Akigusia swala la ajira, Badi alisema kuwa bandari ya Mombasa inazidi kujengwa kila uchao, lakini cha kustaajabisha vijana wa eneo la Pwani na hususan Kaunti ya Mombasa hawajapata nafasi hizo za kazi licha ya kuwa bandari hiyo ni raslimali ya wapwani.
"Wakazi wa Pwani hawana shamba lingine ispokuwa bandari ya Mombasa, kwa hivyo twaiomba serikali kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata kazi katika bandari ya Mombasa ili waweze kujikimu kimaisha na kujiondoa katika maswala ya kipotovu," alisema Badi.
Mbunge huyo amesisitiza kuwepo na mazungumzo ya kina baina wa viongozi wa serikali na wale wa kaunti ili kupata suluhu la kusitisha changamoto zinazowakumba wakazi wa eneo hili la Pwani.