Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya haki za kibinadamu duniani, mashirika mbalimbali ya utetezi wa haki za kibinadamu yamejitokeza na kuikosa serikali kwa kukiuka haki za kibinadamu nchini sambamba na katiba ya nchi.
Mashirika hayo ya kiongozwa na Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini MUHURI yamesema kwamba visa vya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini vimeongezeka kwa asilimia kubwa, huku wengine wakiuwawa na maafisa wa usalama nchini kinyume cha sheria.
Afisa wa haki za kijinsia katika shirika la utetezi wa haki za kibinadamu katika afisa ya umoja wa mataifa Bi Claris Oganga, akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamis alisema kwamba haki za kibinadamu zinafaa kuzingatiwa ili kuona kwamba vita dhidi ya ugaidi, Ardhi na Ufisadi vinafaulu.
"Kuna haja ya serikali kuzingatia haki za kibinadamu nchini ili kuona kwamba haki zote za kijinsia hazikiukwi na kuzua taharuki katika jamii," alisema Oganga mjini Mombasa wakati wa kuadhimisha siku ya haki za kibinadamu duniani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi mkuu wa shirika la MUHURI Hassan Abdille alisema kwamba changamoto wanazopitia ni kutokana na serikali kutoangazia vyema ukomeshaji wa mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na maafisa wa polisi.
"Changamoto tunazozipitia hasa katika mashirika yetu ni jinsi serikali inashindwa kukomesha mauaji ya kiholela yanayotekelezwa na maafisa wa polisi pamoja na watu ambao serikali inawafahamu, lakini iwapo serikali itakuwa inasikiza kauli za mashirika ya kijamii, basi taifa hili litakuwa huru dhidi ya dhulma," alisema Abdille.
Hata hivyo, mkuurgenzi mkuu wa shirika la utetezi wa haki za kibinadamu la Haki Afrika Hussein Khalid aliwataka wananchi kushirikiana vyema na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu ili kuona kwamba dhulma mbalimbali za kibinadamu zinasitishwa.