Share news tips with us here at Hivisasa

Mashirika mbalimbali ya kijamii yameishtumu serikali kutokana na kukithiri kwa kashfa za ufisadi katika idara mbalimbali za serikali humu nchini.

Mashirika hayo ya kiongozwa na Shirika la kutetea haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika, yalisema kwamba serikali imedhihirisha wazi kuwa ilishindwa kudhibiti maswala ya ufisadi nchini, na zaidi kuonekana ikiwatetea baadhi ya maafisa wa serikali wanaokabiliwa na kashfa za ufisadi.

Afisa mpanga ratiba katika Shirika la Haki Afrika Francis Gamba, alisema kwamba Rais Uhuru Kenyatta anafaa kujitokeza waziwazi na kutangaza kukamtwa kwa maafisa wanaoshiriki ufisadi na kufunguliwa mashtaka mahakamani kwa wanaoumia zaidi ni wananchi.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi baada ya kufanya maandamano ya kuishinikiza serikali kuwakabili maafisa wafasadi jijini Nairobi siku ya Jumanne, Gamba alisema kwamba mashirika hayo yatapanga maandamano ya amani kote nchini kuishinikiza serikali na viongozi wa kibinafsi kukoma kufuja mali ya umma.

“Tumepanga kufanya maandamano ya kitaifa kote nchini kuishinikiza serikali na viongozi wengine kukoma kufuja mali ya umma na kuwanyanyasa wakenya wanyonge na badala yake kuungana na kuimarisha uchumi wetu,” alisema Gamba.

Mashirika hayo amepanga kuzuru mashinani na kuwaelimisha wakenya jinsi ya kujiepusha na ufisadi pamoja na kuripoti wanaoshiriki ufisadi na kufuja mali ya umma ili kuona kwamba kwa asilimia kubwa wanaukabili ufisadi.