Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya kitaifa imelaumiwa kwa kuwakabidhi vijana vitambulisho ambao bado hawajafikisha miaka 18 kulingana na katiba ya Kenya.

Hii ni baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya vijana katika Kaunti ya Kisii ambao tayari wako na vitambulisho kabla ya kufikisha miaka 18.

Akizungumza na mwandishi huyu  siku ya Jumatatu mjini Kisii, mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda mjini Kisii Mice Mose alisema kuna baadhi ya vijana ambao wako na vitambulisho kabla ya kufikisha miaka 18, na kukosoa serikali kwa kuwakabidhi vijana hao vitambulisho hivyo.

Kulingana naye, vitambulisho hivyo ndio vimechangia idadi kubwa ya vijana kuacha masomo baada ya kumaliza darasa la nane, na kusema wengi wao wamejihusisha na uendeshaji pikipiki, jambo ambalo si la kufurahisha katika Jamii.

“Naomba serikali ya kitaifa kukoma kuwapa vijana vitambulisho ambao bado hawajafikisha miaka 18 kwani hiyo ni kuhujumu masomo kwa vijana,” alisema Mose.

Wakati huo huo, Mose aliomba wazazi kutowaruhusu watoto wao kuchukua vitambulishoi kabla hawajamaliza masomo ya kidato cha nne kwani masomo ni mhimu.

“Masomo ni ya muhimu katika mmaisha ya leo, bila masomo maisha huwa vigumu naomba kila mzazi kuhakikisha mtoto wake amesoma," aliongeza Mose.

“Kuna wazazi ambao huwanunulia watoto wao pikipiki ili kuendesha kabla ya kumaliza masomo, hilo likomeshwe na wasiruhusie watoto  kushika vitambulisho kabla ya kufikisha miaka 18,” alisistiza Mose.