Askofu kutoka Kisii ameziomba serikali za kaunti na ile ya kitaifa kupambana na visa vya ufisadi ili nchi iweze kusonga mbele.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kisii, Askofu wa kanisa ya Word of Faith Church International Isaac Waire aliomba serikali kukabiliana na visa vya ufisadi ambavyo vimeonekana kuongezeka katika siku za hivi maajuzi.
Kulingana na askofu huyo, ufisadi umeongezeka na kusababisha nchi kurudi nyuma.
Waire aliikosoa serikali kwa kushindwa kuweka mikakati kabambe ya kukabiliana na ufisadi.
Waire alisema kuwa serikali inapaswa kuweka mikakati ya kuzuia ufisadi na kuhakikisha kuwa maafisa wafisadi wanachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Naomba serikali ijaribu kila iwezalo kudhibiti visa vya ufisadi ambavyo vimeongezeka nchini. Hatuwezi songa mbele ikiwa maafisa wa serikali wataendelea kuchukua pesa za wananchi kisiri,” alisema Waire.
Aliongeza, “Hatuwezi kuendelea kuona maafisa wakuu serikalini wakihusishwa na ufisadi. Kenya haiwezi kuendelea iwapo tutashindwa kudhibiti ufisadi serikalini.”
Aidha, askofu huyo alisema serikali inastahili kuunda kamati ya itakayo wachunguza maafisa wafisadi bila mapendeleo.