Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kitaifa imeombwa kuwalipa walimu iliyoajiri kwa miezi mitatu iliyopita kwa njia ya kandarasi baada ya mgomo wa walimu kushuhudiwa nchini.

Hii ni baada ya kubainika kuwa hakuna mwalimu aliyeajiriwa kwa miezi mitatu amepata mshahara wake katika Kaunti ya Kisii.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii wakati walimu hao walienda hadi afisi za kuajiri walimu tawi la Kisii, walimu hao walioajiriwa kwa njia ya kandarasi wakiongozwa na Shadrack Keng’oina walisema hawajakabidhiwa mshahara wao tangu wapate kandarasi na serikali ya kitaifa.

Sasa walimu hao wameomba serikali kuwalipa pesa zao kwani wengi wao wako na familia ambazo huwategemea na hawana chochote cha kutumia kuendesha familia hizo.

“Tangu tuajiriwe hatujawahi pata mshahara kutoka kwa serikali, tunaomba serikali itukabidhi mshahara wetu ili tutumie kulisha familia zetu,” alisema Keng’oina.

“Tulikuwa na kazi ingine tofauti tukakimbilia hii na hakuna pesa tumepata ingawa tuliajiriwa kwa mshahara wa shillingi 30,000 kwa walimu wa sekondari, huku wale wa shule za msingi wakiajiriwa kwa mshahara wa 20,000,” aliongeza keng’oina.

Aidha, walimu hao walikashifu tume ya kuajiri walimu kwa kuwadanganya kuwa ingewaajiri kwa muda wa kudumu, lakini waliandikiwa barua kuwa haitaweza kufanya hivyo, jambo ambalo wamelikashifu zaidi na kusema hiyo ni kuwanyima walimu haki yao.