Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa waendeshaji bodaboda mjini Kisii Mice Mose ameomba serikali kurudisha vikundi vya polisi wa jamii ili kuimarisha usalama kwa wanabodaboda wakati wa usiku jinsi ilivyokuwa hapo mbeleni.

Hii ni baada ya kamishena wa Kaunti ya Kisii Chege Mwangi kuvivunjilia mbali vikundi hivyo vyote katika Kaunti ya Kisii, baada ya kubainika kuwa vikundi hivyo viligeuka na kujifanya kuwa 'polisi'.

Akizungumza siku ya Jumatano mjini Kisii, Mose alisema wakati vikundi vya polisi jamii vilikuwa vinafanya kazi, usalama uliimarika kwa kiasi kikubwa haswa nyakati za usiku ikilinganishwa na siku hizi.

Kulingana na Mose waendeshaji wengi wamekuwa wakijeruhiwa usiku wanapofanya biashara zao za uchukuzi na wengine kunyanganywa pikipiki zao na ata kuawa, jambo ambalo limemfanya kuomba serikali kurudisha vikundi vya polisi jamii ili kushirikiana na maafisa wa polisi kuimarisha usalama usiku.

“Katika siku za hivi maajuzi, tangu polisi jamii ivunjiliwe mbali, visa vya utovu wa usalama vimeongezeka hapa mjini Kisii. Tunaomba polisi jamii kurudishwa ili kushirikiana na polisi kuimarisha usalama kwetu sisi haswa wanabodaboda,” alisema Mose.