Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali kuu na ile ya Kaunti ya Nakuru zimepewa changamoto ya kuimarisha elimu ya vijana ambao hawawezi kugharamia karo za shule kwa kufadhili masomo yao kupitia hazinia mbalimbali kama vile ya CDF.

Wito huu ulitolewa na mkurugenzi wa shule ya upili ya Menengai John Gitau katika kaunti ya Nakuru alipokuwa akihutubu kwenye sherehe ya kuhitimu kwa kundi la vijana wasiojiweza ambao walikamilisha masomo yao ya kiufundi.

Gitau alielezea furaha yake kuona vijana hao wakihitimu na maarifa mbalimbali ikiwemo upishi, usukaji na mengineo.

"Baadhi ya wanafunzi waliohitimu ni walemavu, waliodhalilishwa maishani pamoja na wale wasiojiweza. Vijana hawa sasa wanao uwezo wa kuanzisha biashara yao na hata kuajiri vijana wengine ambao hawana ajira," Gitau alielezea.

Mradi huo ambao unafadhiliwa na hazina ya CDF ya eneo bunge la Bahati husajili vijana wasiojiweza pamoja na akina mama wajane katika masomo mafupi ya miezi minane ambapo wanafunzwa njia za kujikimu maishani.

"Tunaiomba serikali kuu na ya Kaunti ya Nakuru kuendelea kusaidia vijana kama hawa kote nchini kupitia miradi mbalimbali ili wapate njia mbadala ya kujikimu maishani. Pia nawahimiza vijana walemavu kujitokeza na talanta zao na watie bidii katika kuzitumia kuendeleza maisha yao," aliongeza Gitau.

Zaidi ya vijana 220 walihitimu katika sherehe hiyo iliyohudhuriwa na mbunge wa Nakuru magharibi Samuel Arama.