Maskwota wanaoishi katika Shamba la Waitiki lililoko eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, watalazimika kusubiri kujua hatma ya mzozo wa ardhi hiyo baada ya Idara ya Ardhi katika kaunti hiyo kuitaka serikali kuu kusitisha shughuli ya utoaji hati miliki.
Idara hiyo ya ardhi ilisema kuwa inatilia shaka shughuli hiyo, kwa madai kuwa haiendeshwi inavyotakikana.
Akizungumza na wanahabari siku ya Alhamisi mjini humo, kaimu mkuu wa Idara ya Ardhi katika Kaunti ya Mombasa Anthony Njaramba alisema kuwa shughuli hiyo inafaa kusitishwa hadi pale watakapobaini uhalali wa hati miliki hizo.
“Rais alikuja huku mwezi Agosti akapeana hati miliki kwa wakaazi wa Mwakirunge na Ziwa la Ng’ombe, lakini ukiziangalia zinaonyesha kuwa mtu anaishi mahali fulani ambapo ni tofauti na pale mtu huyo anapoishi,” alisema Njaramba.
Njaramba aliongeza kuwa wana wasiwasi kwamba huenda hali kama hiyo ikatokea kwa mamia ya maskwota wanaoishi katika shamba la Waitiki eneo la Likoni.
Aidha, alisema kuwa serikali inafaa kudhibitisha kama kweli shughuli wanayoendesha itakomesha kabisa mzozo huo ambao umedumu kwa muda mrefu.
Kauli hiyo inakuja siku chache baada ya mmiliki wa shamba hilo Evanson Waitiki, kuzuru shamba hilo akiandamana na maafisa wa Idara ya Ardhi na kuwahakikishia wakaazi kwamba amefanya makubaliano na serikali.
Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuzuru Mombasa hivi karibuni kuongoza shughuli hiyo ya utoaji hati miliki kwa maskwota hao.