Serikali kuu imeshinikizwa kuzihudumia shule zote za umma na zile za kibinafsi inapoidhinisha miradi muhimu ya elimu nchini.
Mwenyekiti wa muungano wa shule za kibinafsi nchini yaani ‘Kenya Private Schools Association’, Omar Mbuli amesema kuwa Serikali imeonekana kuwabagua wanafunzi wa shule za kibinafsi na kuwaangazia wale wa shule za umma licha ya kuwa wote wanatumia Mtaala mmoja wa masomo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Mbuli amesema kuwa miradi hiyo ukiwemo ule wa vipakatilishi kwa wanafunzi wa darasa la kwanza unastahili kutekelezwa kwa shule zote za umma na zile za kibinafsi.
“Tunaiomba serikali kuangazia pia shule za kibinafsi wakati wanapoidhinisha miradi muhimu ya elimu nchini kwa sababu sote tunatumia mtaala mmoja wa masomo lakini cha kushangaza wametutenga,” alieza Mbuli.
Wakati uo huo, ameitaka serikali kuwakabidhi wamiliki wa shule za kibinafsi hati miliki za ardhi ili wajikinge na mabwenyenye ambao wamekuwa wakinyakua ardhi zao.
“Tunasema kuwa serikali itutizame nasi pia na itupe hati miliki za ardhi zetu ili kujikinge na baadhi ya mabwenyenye wanaolenga kunya kua ardhi ya shule zetu," aliongeza Mbuli.
Mwenyekiti huyo ameisihi serikali kupunguza ada ya malipo kwa wamiliki wa shule za kibinafsi ya shilingi elfu 54 ambacho amekitaja kuwa kiwango cha juu mno.