Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kutoa usaidizi kwa waendesha bodaboda kwa kuwajengea vibanda ili kuwapa afueni waendeshaji hao kujikinga na mvua inaponyesha na wakati wa jua kali.
Kulingana na waendesha bodaboda hao, hawajafurahi jinsi wanateseka na mvua pamoja na jua kali ili hali hutoa ushuru kila mwezi na hawaoni mafanikio ya ushuru huo kwani hakuna kibanda ata kimoja kimejengwa mjini Kisii.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu mjini Kisii, waendeshaji wa bodaboda mjini humo wakiongozwa na Joseph Mogambi, ambaye ni mwenyekiti wa shirika la waendesha bodaboda mjini humo aliomba serikali ya kaunti hiyo kuwajengea vibanda ili kuwasaidia.
Mogambi alisema hawafurahii jinsi serikali ya kaunti ilivyoandika ripoti kuwa serikali ya kaunti imejenga vibanda kwa waendesha bodaboda mjini Kisii huku wakisema hakuna kibanda kimejengwa mjini humo.
“Naomba serikali iwache kuwadanganya wananchi kuwa imejenga vibanda kwa waendesha bodaboda mjini Kisii hakuna kibanda kimejengwa hadi sasa,” alisema Mogambi.
“Tunaomba kaunti yetu ijenge vibanda mjini Kisii ili nasi tufurahie matunda ya serikali za ugatuzi,” aliongeza Mogambi.
Matamshi hayo yaliungwa mkono na wanabodaboda wengine ambao wanaomba kaunti kuwapa usaidizi.