Siku moja tu baada ya Afisa wa KDF kumpiga risasi na kumuuwa mwanamume wa umri wa miaka 25 anayedaiwa kuwa na akili tairi, mashirika ya utetezi wa haki za kibinadamu yamejitokeza kukashfu mauaji hayo.
Afisa mratibu wa mipango katika shirika la Haki Afrika Francis Auma Gamba alisema kuwa muungano wa mashirika ya kutetea haki za kibinadamu na yale ya kijamii yanataka uchunguzi wa haraka kufanywa dhidi ya mauaji hayo na ripoti kamili kutolewa.
Gamba alisema kuwa hatua ya afisa huyo kumpiga risasi mwanamume huyo na kumua ni ukiukaji wa haki za kibinadamu kwani kama afisa wa usalama angefaa kumtia nguvuni iwapo anamshuku kuwa mhalifu.
Alisema kuwa visa vya maafisa wa usalama kuwauwa Wakenya kiholela imekuwa kama tabia na lazima hatua kali dhidi ya wahusika kuchukuliwa ili kuokoa Wakenya wasiokuwa na hatia kwani kizazi kijacho huenda kikaathirika kufuatia kushuhudia visa hivyo.
"Tunataka haki itendewe familia ya jamaa huyo na hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya afisa huyo wa KDF ili kuona kwamba visa vya mauaji ya kiholela vinasitishwa humu nchini," alisema Gamba wakati akizungumza na wanahabari katika eneo la tukio siku ya Jumatano.
Mwanaharakati huyo wa kutetea haki za kibinadamu nchini ameipa serikali makataa ya siku saba kueleza bayana kiini halisi cha mauaji hayo kwani kulingana na mashirika hayo ya kijamii afisi huyo wa KDF alikusudia kumua jamaa huyo.