Mashirika ya kijamii ya Haki Afrika na Muhuri yameipa serikali makataa ya siku saba kuwachukulia hatua maafisa wa jeshi la KDF waliomuua kwa kumpiga risasi mwanaume mmoja katika eneo la Likoni Mombasa siku ya Jumatano.

Share news tips with us here at Hivisasa

Afisa mratibu wa Haki Afrika, Francis Auma, ameitaka serikali kufafanua kwanini wanajeshi hao waliamua kumuua Ndomo Mwembe mwenye umri wa miaka 25, anayesemakana kuwa na akili taahira badala ya kumtia nguvuni.

Akizungumza katika eneo la Mtongwe siku ya Alhamisi alipoitembelea jamii ya marehemu, Auma aliwalaumu maafisa hao na kuwashutumu kwa kutumia nguvu kupita kiasi, huku akiutaja mauaji hayo kama ukiukaji mkubwa wa sheria na haki za binadamu.

''Mtu asiye na akili timamu unammimia risasi badala ya kumkamata, si haki hata kidogo,'' alisema Auma.

Auma sasa anaitaka serikali kuwakamata maafisa hao na kuwafungulia mashtaka ya mauaji ya kusudia.

Kauli yake imeungwa mkono na mwakilishi wa wadi ya Mtongwe ambaye anadai maafisa wa KDF wamekuwa wakiwadhulumu na kuwatesa wenyeji wasio na hatia kwa muda sasa.

Siku ya Jumatano, Ndomo Mwembe, mwenye akili taahira aliuwawa baada ya kupigwa risasi na maafisa wa jeshi la KDF katika eneo la Mtongwe, Likoni kwa madai ya kulishambulia kwa mawe gari la maafisa hao.