Serikali ya Kaunti ya Mombasa imehimizwa kupiga marufuku vilabu vinavyofunguliwa kila uchao katika maeneo ya Kisimani na Bombolulu huko Kisauni, mjini Mombasa.
Wakazi wanaoishi katika maeneo hayo wamesema kwamba kumekuwepo na ongezeko la baa na vilabu na maeneo ya kuuza pombe ya mnazi katika sehemu za makazi, hali ambayo huwatatiza katika hali yao ya maisha kila uchao.
Wakiongozwa na afisa wa polisi jamii katika eneo la Kisimani Abdallah Abdulraham, wakazi hao wameitaka serikali ya Kaunti ya Mombasa kushirikiana na maafisa wa utawala katika eneo hilo ili kuvifunga vilabu na baa hizo.
Akizungumza siku ya Ijumaa katika eneo hilo la Kisimani, Abdulrahman alisema kwamba vilabu hivyo na baa za pombe zimesababisha utovu wa maadili miongoni mwa jamii ya eneo hilo, huku visa vya ubakaji, utumizi wa dawa za kulevya na wizi miongoni mwa maovu mengine vikiongezeka katika maeneo ya Bombolulu na Kisimani.
“Ni lazima serikali ya Kaunti ya Mombasa ishirikiane na maafisa wa utawala katika eneo hili la Kisimani ili kuzia ulevi wa kupindukia,” alisema Abdulrahman.
Hapo awali, Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita alizindua oparesheni ya kuvifunga vilabu vilivyokuwa vikiendeleza shughuli zake bila leseni, japo bado vilabu vipya vya pombe vimekuwa vikiongezeka katika eneo zima la Kisauni.