Serikali imehimizwa kukabiliana na swala la utumizi wa dawa za kelevya miongoni mwa vijana..
Kulingana na afisa wa nyanjani katika shirika la Kenya Harm Reduction, Caleb Angira, zaidi ya vijana elfu 26 katika ukanda wa pwani wameathirika na utumizi wa dawa za kulevya licha ya mashirika mbali mbali ya kijamii kuwashauri vijana kujitenga na mihadarati.
Angira alisema kuwa utafiti uliofanywa na shirika hilo ulibaini kuwa asilimia 18.2 ya vijana wanaotumia dawa za kulevya nchini wameathirika na virusi vya ukimwi kutokana na utumizi wa sindano moja.
Akizungumza katika kongamano la kiafya mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Angira alisema kwamba ni lazima kwa serikali kujitokeza waziwazi na kuangamiza dawa hizo huku waathiriwa wakipelekwa katika vituo vya kurekebisha tabia waraibu wa mihadarati.
Angira ameitaka serikali kubuni mbinu mbadala za kuwatia nguvuni walanguzi wakuu wa mihadarati humu nchini kwani wanachangia pakubwa katika kuathirika kwa vijana wadogo.
Angira aliwakosoa baadhi ya maafisa wakuu wa idara ya usalama kwa kuwaacha huru walanguzi hao.
“Vijana wengi walioathirika na utumizi wa dawa za kulevya wameambukizwa virusi vya ukimwi. Utafiti tuliofanya umebaini kuwa asilimia 18.2 wameabukizwa ukimwi hali ambayo inahitaji kushughulikiwa kabla ya vijana wengi kupotoka,” alisema Angira.
Aidha, amewataka viongozi wakuu serikalini, wanaharakati wa kupambana na mihadarati na vitengo vya usalama kubuni vikao vya dharura ili kulijadili jinsi watakavyokabiliana na janga hilo kabla ya kupoteza idadi kubwa ya vijana hususana katika eneo la pwani.