Serikali kuu imeshinikizwa kutenga hazina maalum itakayotumiwa na wawakilishi wa kike katika kila Kaunti nchini ili kutekeleza mikakati ya kimaendeleo mashinani.
Kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake kaunti ya Mombasa Bi Afiya Rama, hakuna hazina maalum inayowawezesha viongizi hao kutekeleza shughuli za kimaendeleo ikilinganishwa na wabunge ambao wana fedha za hazina ya CDF.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Bi Afiya alisema kwamba wawakilishi wa kaunti wanahitaji hazina maalum ili waidhinishe miradi mbalimbali ya kijamii na kulikabili tatizo la dhuluma za kijinsia.
Bi Afiya anapendekeza kwamba maseneta wanapaswa kuwekeza hazina maalum ili wajishughulishe na maswala ya kimaendeleo mashinani, licha ya wengi wao kuwajibika bado hawana hazina za kifedha.
“Kuna haja ya serikali kutenga hazina maalum kwa wawakilishi wa wanawake nchini ili kuwawezesha kuwa na nafasi ya kuwatekelezea wananchi miradi mbalimbali ya kimaendeleo,” alisema Bi Afiya.
Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi na mipango ya Kitaifa Bi Anne Waiguru alisema kwamba shilingi bilioni mbili zitakuwa zikitengwa kila mwaka ili kuwawezesha wawakilishi wa kike kuendeleza miradi ya kijamii mashinani, lakini fedha hizo hazijasambazwa hadi sasa.