Mbunge wa Lugari Ayub Savula ameitaka serikali kuu ikiongozwa na rais Uhuru Kenyatta pamoja na tume ya uwiano na utangamano nchini NCIC, kuzindua mpango wa uwiano wa kitaifa kabla ya uchaguzi wa 2017.
Akiongea mjini Nakuru Jumapili, Savula alisema kwamba matokeo ya wakimbizi wa ndani kwa ndani kutoka Nyandarua na Nakuru kuandamana wakati ambapo naibu wa rais anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya uhalifu wa jinai ICC Hague Uholanzi, yanaipa mahakama hiyo picha ‘isiyopendeza’ kuhusu hatma ya wakimbizi hao.
Aliichangamoto serikali ya Jubilee kuharakisha mpango wa kuwafidia wakimbizi hao pamoja na kuwapa makao.
“Serikali ya Uhuru Kenyatta iwape mara moja makao, na fidia. Matokeo ya wiki jana hayavutii hata kidogo, IDPs kuandamana wakati naibu rais na Joshua Sang wana kesi hiyo,” Savula alisema.
Kulingana na Savula, Kenya imeendelea kushuhudia amani baada ya matukio ya 2017, na hivyo kuna haja ya kesi dhidi ya Ruto na Sang kutamatishwa kwa manufaa ya Kenya.